Mahakama ya Upeo Kenya leo inaanza kusikiliza kesi ya kupinga kutangazwa kwa William Ruto kuwa Rais Mteule.
Pande husika zimetoa madai ya kila aina na hivyo majaji saba wa mahakama hiyo ya kilele watakuwa na kibarua kigumu kutofautisha kati ya ukweli, porojo na uongo ili kuamua kesi hiyo kwa haki bila ushawishi wowote kutoka nje. Katika kikao cha leo, mahakama hiyo itaweka wazi kanuni na taratibu zitakazofuatwa na pande zote katika mahakama hiyo.
Mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya Muungano wa Azimo One Kenya Raila Odinga anaitaka Mahakama ya Upeo kutupilia mbali ushindi wa William Ruto wa Muuungano wa Kenya Kwanza au kumtangaza yeye kama mshindi katika uchaguzi wa rais wa tarehe tisa mwezi Agosti huku mojawapo ya kesi zilizowasilishwa mahakamani humo ikidai kwamba hakuna yeyote kati ya wawili hao aliyepata asilimia hamsini na kura moja. Odinga ambaye ni mwanasiasa mkongwe mwenye umri wa miaka 77 alisema makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliyompatia ushindi mshindani wake mkuu William Ruto.
Makamishna wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi IEBC wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti, Juliana Cherera walijitenga na matokeo hayo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume Wafula Chebukati, wakidai kwamba marhala ya mwisho ya mchakato wa kuyatangaza haikuwa na uwazi. Mwenyekiti wa IEBC alimtangaza William Ruto mshindi wa uchaguzi wa rais, kwa kuapata kura milioni 7.1, sawa na asilimia 50.49 ya kura milioni 14 zilizopigwa, huku Raila akiambulia kura milioni 6.9, sawa na asilimia 48.85 ya kura. Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Mahakama ya Upeo inatazamiwa kutangaza maamuzi yake Jumatatu Septemba tano.