Raisi: Kuimarishwa uhusiano wa Saudi Arabia na Iran ni kwa maslahi ya usalama wa eneo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ubunifu na hatua za Iraq katika kuboresha ushirikiano baina ya nchi za eneo bila uingiliaji wa madola ajinabi ni jambo ambalo limekuwa na taathira na kuongeza kuwa: “Kurekebishwa na kuimarishwa uhusiano wa Iran na Saudi Arabia ni kwa maslahi ya usalama wa eneo.”

Kwa mujibu wa taarifa, Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Jumatatu usiku wakati alipokutana na kuonana na Fouad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ambapo ameishukuru serikali ya Iraq kutokana na kufanya mazungumzo na mashauriano kuhusu masuala ya eneo na kuongeza kuwa: “Hatua za Iraq katika kuboresha mazingira ya ushirikiano baina ya nchi za eneo bila kuwepo uingiliaji wa madola ajinabi ni jambo mbalo litakuwa na taathira chana katika kuimarisha ushirikiano wa kieneo.”

Raisi amesema duru tano za mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia kwa upatanishi wa Iraq zimekuwa ni zenye manufaa na kusisitiza kwamba kwa kutekelezwa mpapatano yaliyopita, kutachukuliwa hatua za kuinua kiwango cha uhusiano.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema uthabiti unaweza kurejea Iraq kwa njia ya mazungumo tu baina ya makundi ya kisiasa nchini humo na kwa msingi wa katiba ili kuandaa mazingira ya kuundwa serikali mpya ambayo itatatua matatizo ya Wairaqi. Aidha amesisitiza kuwa nafasi ya Marajii wa kidini ni muhimu sana Iraq.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amepongeza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuleta uthabiti na usalama nchini Iraq na ukamilishaji wa mchakato wa kisiasa wa kuundwa serikali mpya nchini humo. Aidha  katika kikao hicho amemkabidhi rais wa Iran ripoti ya nafasi ya Iraq katika kuboresha uhusiano wa Iran na Saudi Arabia.

Kabla ya hapo pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *