IRGC ya Iran yaeleza ilivyotwaa na kuachia huru droni ya Marekani

Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa maelezo ya kina kuhusu namna lilivyoteka na kisha kuachia huru ndege isiyo na rubani ya baharini ya Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

IRGC imefafanua kuwa, imetoa maelezo hayo ili kujibu madai ya kuchekesha ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi, dhidi ya Vikosi vya Baharini vya jeshi la SEPAH.

Taarifa ya IRGC imebainisha kuwa, droni hiyo ya Marekani ambayo ilikuwa imepoteza mawasiliano, ilinaswa na kudhibitiwa na Vikosi vya Baharini vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ili kudhamini usalama wa njia za baharini zinazotumiwa na meli za mizigo na mafuta.

IRGC imeeleza kuwa, vikosi vyake vya majini vililazimika kuchukua hatua hiyo ili kuzuia kutokea ‘ajali’ yoyote, wakati huu ambapo kesi kadhaa za uharamia zimeripotiwa katika eneo hili katika wiki za karibuni.

Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limeeleza bayana kuwa, droni hiyo ya Marekani iliachiwa huru baada ya Wamarekani kukiri kuwa walikuwa wamefanya makosa, na kuthibiti kuwa chombo hicho hakikuwa hatari kwa usalama wa taifa la Iran.

Jeshi la IRGC kadhalika limelionya vikali jeshi la majini la Marekani na kulitaka lisirudie tena vitendo vya aina hiyo vinavyokanyaga sheria.

SEPAH ya Iran imeongeza kuwa, uwepo wa vikosi vya kigaidi vya Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni tishio kwa usalama na uthabiti wa eneo hili la kistratajia.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *