Umoja wa Mataifa umetoa ripoti inayoeleza kufanyika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur katika jimbo la Xinjiang nchini China.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet imeeleza kuwa, madai ya mateso ni kweli na kuna uwezekano kwamba kulifanyika uhalifu dhidi ya binadamu. Ripoti hiyo inaibua uwezekano wa “uhalifu dhidi ya ubinadamu” na inataja “ushahidi wa kuaminika” wa mateso na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watu wa jamii ya Uighur walio wachache na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua haraka.
Sehemu moja ya ripoti hiyo inasema kuwa, kiwango cha visa vya kuzuiliwa kiholela na ubaguzi dhidi ya watu wa jamii ya Uighur na makundi mengine ya Waislamu ni kikubwa na kinaweza kuwa uhalifu wa kimataifa, hasa uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Katika radiamali yake kwa ripoti hiyo, serikali ya China imesema kuwa, ripoti hiyo imetegemea habari za uongo zilizotungwa na maadui wa China na kwamba, huo ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya China.
Kwa muda sasa asasi mbalimbali zimekuwa zikilaani ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali ya China dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur katika jimbo la Xinjiang kaskazini mwa China na kusema kuwa, ukandamizaji huo mkubwa haujawahi kushuhudiwa nchini humo.
Hata hivyo serikali ya China imekuwa ikikana tuhuma dhidi yake za mateso dhidi ya Waislamu, ikisema kuwa inawapatia mafunzo katika kambi ili waondokane na fikra za itikadi kali. Wauighur wanaishi kaskazini magharibi mwa China katika jimbo lenye mamlaka yake ya ndani la Xinjiang.