Yemen: Tuna uwezo wa kupiga popote katika maji yanayoizunguka nchi yetu

Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, nchi hiyo ina uwezo wa kupiga na kushambulia katika sehemu yoyote ya maeneo ya majini yaliyoko karibu na Yemen.

Televisheni ya Almasirah imetangaza habari hiyo leo Ijumaa na kumnukuu Mahdi al Mashat akisema hayo wakati wa gwaride kubwa la kijeshi lililofanyika kwenye mkoa wa al Hudaidah wa magharibi mwa Yemen na kuziambia nchi vamizi kwamba: Nyinyi nchi vamizi ndio mnaohatarisha usalama wa safari za vyombo vya habarini katika maji ya kimataifa. Vitendo vyenu vya kinyama vinasababisha mateso na maumivu makubwa kwa wananchi wa Yemen.

Itakumbukwa kuwa mwezi Machi 2015, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ziliongoza muungano vamizi wa nchi za Kiarabu katika kuanzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen kwa msaada na baraka kamili za Marekani na nchi za Ulaya kama ambavyo inaaminika pia kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel nao uko mstari wa mbele kuyasaidia kwa hali na mali madola hayo vamizi.

Tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hizo vamizi zimeizingira Yemen kutokea ardhini, majini na angani. Lakini wananchi wa Yemen kupitia jeshi lao na vikosi vya kujitolea vya wananchi maarufu kwa jina la Ansarulah, wameweza kusimama imara kuilinda nchi yao na kutoa pigo kubwa kwa wavamizi.

Vile vile televisheni hiyo ya Almasirah imemnukuu al Mashat akiwaambia wavamizi hao kwamba, meli zenu za kivita mlizoziweka karibu na nchi yetu kwa ajili ya kutuzingira na kufanya uharibifu, hazimtishi hata mtoto mdogo wa Yemen.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *