Msemaji wa Ofisi ya Kisiasa ya Taliban nchini Qatar amesema kuwa, kundi hilo halina mpango wa kuutambua rasmi utawala haramuu wa Israel.
Mulla Muhammad Naeem amekanusha taarifa za baadhi ya vyombo vya habari vinavyoeleza kwamba, kundi la Taliban halina tatizo na nchi yoyote ile ukiwemo utawala ghasibu wa Israel na kubainisha kwamba, amenukuliwa vibaya kwani huo siyo msimamo wa Taliban.
Mulla Muhammad Naeem ameongeza kuwa, msimamo wa serikali ya Taliban ya Afghanistan kuhusiana na Beitul-Muqaddas uko wazi na bayana na kwamba, Taliban imebainisha msimamo huo na kuukariri mara kadhaa.
Msemaji wa Ofisi ya Kisiasa ya Taliban nchini Qatar ameeleza kwamba, Beitul-Muqaddas ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kitu chenye thamani kwa Waislamu wote na kwamba, inachokifanya Israel huko Palestina ni dhulma kubwa na ukandamizahji wa wazi hivyo sisi hatuwezi kuwa pamoja na dhalimu hata kwa lahadha moja.
Amesisitiza kuwa, suala siyo kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel au kuwa na uhusiano nao kwani hilo ni jambo ambalo halimo kabisa katika sera za Taliban hasa kwa kutilia maanani kwamba, siasa za utawala wa Taliban zinazingatia sheria za Kiislamu na maslahi ya kitaifa ya Afghanistan.