Mkuu wa zamani wa majeshi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Shaul Mofaz amesema, Wairani ni watu werevu sana na wanao uwezo wa kuhakikisha wanapata haki zao za kinyukilia; na akakiri kwa kusema, Tel Aviv haina uwezo wa kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Tehran.
Mofaz ameyasema hayo katika mahojiano na Kanali 12 ya Televisheni ya utawala huo ghasibu na kubainisha kwamba, ni jambo lililo mbali kwa Israel kuweza kuchukua hatua ya upande mmoja ya kijeshi dhidi ya Iran na akafafanua kuwa, hatua ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran ina maana ya kuanza vita vya kieneo; na Israeli haiwezi kuingia katika vita kama hivyo peke yake.
Mkuu huyo wa zamani wa majeshi ya utawala wa Kizayuni ameeleza hayo, wakati hivi karibuni gazeti la Kiebrania la Haaretz liliripoti kuwa, wanasiasa na maafisa wa kijeshi wa Israel wamewadanganya watu wao na fikra za waliowengi kwa kudai kwamba, Tel Aviv imeshajiweka tayari kitambo kwa ajili ya kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, kwa sababu kama ni kweli Israeli ilikuwa na chaguo hilo, ingepasa ilitekeleze mara baada ya Iran kuanzisha mpango wake wa nyuklia.
Haaretz limetilia shaka uwezo wa utawala wa Kizayuni wa kutumia chaguo la kijeshi kushambulia mpango wa nyuklia wa Iran na kuongeza kuwa, yumkini viongozi wa Israel wanategemea uwezo wa kijeshi ambao kiuhalisia hauko kwenye mamlaka yao.