Viongozi kadhaa wa kidini, kisiasa, wanafikra na wasomi wa Kipakistan wamesema katika kongamano la kifikra kuhusu Palestina kwamba, juhudi za hivi karibuni za Marekani na vibaraka wake za kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Pakistan na Israel zimegonga mwamba.
Mkutano wa Kamati ya Kuunga Mkono Jumuiya ya Palestina nchini Pazkistan ulifanyika Ijumaa iliyopita ya Septemba Pili na kuhudhuriwa na wasomi na wanafikra akiwemo Amir Muslim Parviz, Naibu Mkuu wa Jamaat Islami, Allama Kadhi Ahmad Noorani, mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Maulamaa wa Pakistan na viongozi kadhaa kutoka vyama kadhaa vya kisiasa kama Muslim League Nawaz, Takreek Insaf na Harakati ya Muungano wa Kikaumu na kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya hivi karibuni yanayohusiana na muqawama wa Palestina pamoja na mbinu na mikakati ya kukabiliana na njama za kila upande za madola ya Magharibi zinazolenga kusukuma mbele mpango mchafu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida mataifa ya Kiislamu hususan Pakistan na utawala wa kibaguzi wa Israel.
Wanafikra na wasomi hao wa Kipakistan sanjari na kusisitizia udharura wa kuendelezwa muqawama na mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kutetea malengo matukufu ya wananchi madhlumu wa Palestina, wamesisitiza himaya na uungaji mkono wao wa kila upande wa Waislamu wa Palistan kwa makundi ya muqawama wa Palestina katika kukabiliana na hujuma za kijeshi za utawala dhalimu wa Israel.
Kufanyika mkutano wa kifikra wa wasomi wa Pakistan kwa minajili ya kuweka wazi siasa za majitaka za Marekani katika eneo la Asia Magharibi na njama za utawala ghasibu wa Israel ni ishara ya wazi kwamba, Maulamaa wa Pakistan wanafuatilia kwa karibu nyendo za Marekani na Israel na kwamba, wana uwezo kukabiliana na njama za maadui dhidi ya mataifa ya Kiislamu.
Tukitupia jicho kwa haraka haraka sera na siasa za Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika eneo hususan nchini Afghanistan unadhihirika ukweli na uhakika huu kwamba, baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini Afghanistan, Washington imekabiliwa na hali mbaya. Viongozi wa Marekani walikuwa wakidhani kwamba, baada ya kuondoka Afghanistan wangeweza kupeleka wanajeshi wao katika matiafa ya Asia ya Kati au nchini Pakistan. Hata hivyo dhana yao hiyo kama zilivyo ndoto zao nyingine za alinacha za viongozi wa White House ilikabiliwa na changamoto na vizingiti lukuki.
Viongozi wa mataifa ya Asia ya Kati walitangaza kinagaubaga upinzani wao dhidi ya hatua ya Marekani ya kuleta wanajeshi wake hata kwa muda tu katika mataifa yao. Aidha nchini Pakistan siasa za Marekani zimekabiliwa na mkwamo. Ukweli wa mambo ni kuwa, ukiondoa wanasiasa wachache wanaoiunga mkono Marekani katika uga wa siasa za Pakistan, akthari ya wanasiasa wa nchi hiyo na wananchi Waislamu wa Pakistan wanapinga vikali ushirikiano wa aina yoyote ile wa nchi yao na Marekani pamoja na utawala ghasibu wa Israel.
Baada ya Marekani na washirika wake kushindwa katika njama zao za kuanzisha vita baina ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni, kuliandaliwa mpango maalumu wa kufanya safari huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu wanasiasa wa Pakistan wenye uraia pacha. Hata hivyo, wanasiasa wa Pakistan walitoa radiamali hasi pia kwa njama hii ya Marekani na kufanya ufichuaji katika uwanja huo.
Kwa mfano, Ahsan Iqbal, Waziri wa Ustawi na Mipango wa Pakistan akitoa radiamali yake kwa tetezi zilizoibuka baada ya safari ya hivi karibuni ya ujumbe wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwamba, baadhi yao walikuwa ni Wapakistan wenye uraia pacha ametangaza kuwa:
Hakuna ujumbe wowote ule uliotumwa na serikali ya Pakistan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na siasa zetu kuhusiana na kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel hazijabadilika.
Aidha mwanasiasa huyu amesisitiza kuwa: Sera za serikali ya Islamabad ziko wazi na zinazoeleweka. Serikali ya Pakistan katu haiwezi kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel, bali inawaunga mkono kaka na dada zake Waislamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wenye ghamu na huzuni.
Imran Khan, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan naye alikosoa Aprili mwaka huu katika hadhara ya wafuasi wa chama chake katika mji wa Charsadda kuhusu safari ya ujumbe huo huko Israel na kutahadharisha kuhusiana na hatua yoyote ile ya kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.
Allama Raja Nasir Abbas, Katibu Mkuu wa chama cha Majlis Wahdat-e-Muslimeen Pakistan naye sambamba na kutoa taarifa inayolaani kuandamana na ujumbe wa Marekani baadhi ya raia wa Pakistan waliohadaiwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu amesema:
Ni marufuku kufanya urafiki na kulegeza msimamo kwa namna yoyote mbele ya Israel inayofanya mauaji, na kufanya hivyo kunahesabiwa kuwa ni khiyana na usaliti kwa mwasisi wa Pakistan. Hivyo, basi kuna haja kwa serikali ya Islamabad kuwa macho na aina yoyote ile ya njama za kutaka kuweko uhusiano wa kawaida baina ya taifa hilo na utawala haramu wa Israel.
Radiamali kali za viongozi wa Islamabad na wanasiasa wa Pakistan kwa raia kadhaa wa Pakistan waliohadaiwa ambao waliandamana na ujumbe wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni ishara ya wazi ya ukweli na uhakika huu kwamba, serikali na wananchi wa Pakistan hawana hamu wala shauku ya kuona nchi yao inaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel. Pamoja na hayo, Israel ikisaidiwa na Marekani inafanya njama za kuwadaa baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiislamu na kuonyesha kwamba, upinzani dhidi ya Israel unaishia katika nchi kadhaa chache tu katika ulimwengu wa Kiislamu.
Licha ya hali kuwa hivyo, lakini tukiachana na baadhi ya viongozi waliohadaiwa katika baadhi ya mataifa ya Kiislamu, ukweli wa mambo ni kuwa, tawala za Kiislamu na wananchi wa mataifa ya Kiislamu hawataki kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel na kivitendo wanafanya kila wawezalo kuwa mbali na utawala huo unaofanya mauaji kila uchao dhidi ya Wapalestina.
Pakistan ni mfano mmoja tu wa upinzani dhidi ya Israel. Nchini Afghnaistan licha ya kuweko vitisho na mashinikizo ya Marekani, lakini serikali ya wanamgambo wa Taliban imetangaza kuwa, haina mpango wa kuanzisha uhusiano na Israel au kuutambua rasmi utawala huo ghasibu, na badala yake inaunga mkono malengo na misimamo ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.