Kombe la Dunia la Qatar 2022 litakuwa la kihistoria kwa mchezo wa soka barani Afrika, kwa sababu nchi zote tano za bara hilo zinazoshiriki katika michuano ya kuwania kombe hilo ambazo ni Morocco, Senegal, Cameroon, Tunisia na Ghana zitaongozwa na makocha Waafrika.
Kwa mujibu ripoti ya toleo la leo la gazeti la Kayhan, kocha Mbosnia Vahid Halilhodzic amejiuzulu uongozi wa timu ya taifa ya Morocco, na badala yake Walid Al-Rakraki, mchezaji wa zamani wa timu hiyo, ametangazwa kuwa kocha mkuu mpya. Kwa hatua hiyo na katika tukio la kihistoria kwa bara la Afrika, makocha wakuu wote wa timu za bara hilo katika Kombe la Dunia mwaka huu watakuwa ni wazawa.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeeleza kwamba, hatua hiyo ni mabadiliko muhimu katika maendeleo ya makocha wa Kiafrika ambao sasa wana ujasiri na ushujaa wa kuzinoa na kuziongoza timu za mataifa yao katika ngazi ya juu kabisa.
Mechi za hatua ya makundi za Kombe la soka la Dunia la Qatar 2022 zitafanyika kuanzia Novemba 20 hadi Desemba 2, hatua ya timu16 itaanza Desemba 3 hadi 6, robo fainali itafanyika Desemba 9 na 10, nusu fainali tarehe 13 na 14 za mwezi huo, na fainali ya mashindano hayo itafanyika tarehe 18 Desemba.