Rais wa Burundi amtimua Waziri Mkuu kufuatia tetesi za mpango wa mapinduzi

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amemfuta kazi waziri mkuu wake, Alain Guillaume Bunyoni baada ya kuonya kuhusu njama ya “mapinduzi” dhidi yake.

Ndayishimiye amemfuta kazi Guillaume Bunyoni na mkuu wa baraza lake la mawaziri, Jenerali Gabriel Nizigama, katika siku ya taharuki kubwa kwenye nchi hiyo yenye machafuko ya Afrika ya Kati.

Alain Guillaume Bunyoni alikuwa mmoja wa watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya serikali ya Rais Ndayishimiye.

Hatua hii ya Ndayishimiye imechukuliwa siku chache baada ya kiongozi huyo kuwashutumu hadharani wale aliosema kuwa “wanajiamini kuwa wana nguvu zote” na wana ndoto ya kushika madaraka kupitia mapinduzi.

Katika kikao cha Bunge la Burundi kilichoitishwa kwa haraka, wabunge wameidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Usalama, Gervais Ndirakobuca, kuchukua nafasi ya Bunyoni kama Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.

Hatima ya Bunyoni, ambaye ni mmoja wa viongozi wa ngazi za juu katika chama cha CNDD-FDD, kundi la zamani la waasi ambalo limetawala nchi hiyo maskini kwa miaka mingi, haikujulikana mara moja.

Nafasi ya mkuu wa baraza la mawaziri, Jenerali Gabriel Nizigama pia imechukuliwa na Kanali Aloys Sindayihebura, ambaye hadi sasa alikuwa akisimamia Idara ya Taifa ya Upelelezi.

Ndayishimiye alichukua madaraka mnamo Juni 2020 baada ya mtangulizi wake, Pierre Nkurunziza, kufariki dunia kutokana na kile mamlaka ya Burundi ilisema ni mshtuko wa moyo.

Kuchaguliwa kwake mwezi Mei 2020 kulitoa matumaini ya hali bora kwa kiasi fulani baada ya utawala wa machafuko na umwagaji damu wa mtangulizi wake, ingawa Burundi imeshindwa kuboresha rekodi yake mbaya kuhusu haki za binadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *