Ugiriki yaonya juu ya kutokea vita vingine barani Ulaya sawa na vya Ukraine

 

Waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki ametoa indhari ya kutokea vita vingine barani Ulaya kama vya Ukraine na kusisitiza kuwa iwapo Uturuki itaanzisha mashambulizi, Ugiriki itachukua hatua ya kujihami.

Shirika la habari la Fars limeripoti leo kuwa, serikali ya Ugiriki imewaandikia barua washirika wake katika NATO, Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuwataka walaani rasmi maneno ya kuzusha mvutano yaliyotolewa na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki.
Katika barua hizo, waziri wa mambo ya nje wa Ugiriki Nikos Dendias amesema, mwenendo wa Uturuki inapasa ukosolewe na kulaumiwa na taasisi hizo tatu.
Akizungumzia vita vya Ukraine kwa lugha ya mafumbo, Dendias amefafanua kwa kusema: “kwa kutofanya hivyo kwa wakati au kwa kudharau uzito wa suala hilo, kuna hatari ya kukabiliwa na hali sawa na ile inayoendelea kushuhudiwa hivi sasa katika sehemu zingine za bara letu; ni kitu ambacho hakuna yeyote kati yetu anayetamani kukiona.”

Siku ya Jumanne, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki aliitishia tena Ugiriki; nayo Ugiriki ikajibu kwa kutangaza kuwa iko tayari kujihami. Rais wa Uturuki alisema, Uturuki inaweza usiku mmoja ikaelekea ghafla Ugiriki.

Katika barua kwa Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Athens imeashiria maneno aliyotamka Erdogan kuhusiana na kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu visiwa vya Ugiriki katika Bahari ya Aegean.
Uturuki na Ugiriki zinatofautiana katika masuala mengi. Masuala ya uhamiaji, madai ya umiliki wa ardhi na ushindani wa kijeshi ni miongoni mwa mambo yaliyoufanya uhusiano wa nchi hizo mbili jirani ugubikwe na wingu zote la mvutano.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *