Mamia ya wananchi wa Morocco wameandamana kulaani utovu wa kimaadili wa balozi wa utawala haramu wa Israel mjini Rabat ambaye anakabiliwa na kashfa ya ngono.
Waandamanaji wenye hasira wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara dhidi ya utawala haramu wa Israel na kutoa mwito wa kufanyika uchunguzi kuhusiana na kashfa ya ngono inayomkabili balozi wa Israel nchini Morocco.
Maandamandamano hayo yamefanyika siku chache tu baada ya Israel kumuita nyumbani David Govrin balozi wake mjini Rabat kwa ajili ya uchunguzi kufuatia taarifa zilizoenea kwamba, amekuwa akijihusisha na vitendo vya utovu wa maadili.
Ripoti kutoka Morocco zinasema kuwa, balozi huyo wa Israel anakabiliwa na tuhuma kadhaa za kuwatumia vibaya wanawake, kuwakabaka na kuwanyanyasa.
Aidha balozi huyo wa utawala ghasibu wa Israel anakabiliwa na tuhuma kadhaa za ufisadi na ubadhirifu na tayari uchunguzi umeanzishwa ambapo miongoni mwa kashfa za ufisadi anazokabiliwa nazo ni kupotea kwa zawadi ya Mfalme wa Morocco ambayo alipatiwa kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel na hakuikabidhi zawadi hiyo kwa Baraza la Mawaziri la Israel.
Waandamanaji hao wamelaani pia hatua ya nchi yao ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina.
Disemba mwaka 2020 Morocco ilijiunga na UAE, Bahrain na Sudan katika kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani. Mapatano hayo yanaendelea kulaaniwa ndani ya nchi hizo za Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.