Jihadul Islami: Jinai za Israel zinazidisha ari na irada ya muqawama

Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imetangaza kuwa, jinai za utawala ghasibu wa Israel zinazidisha ari na irada ya muqawama na mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala huo ghasibu.

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Jihadul-Islami imepongeza operesheni ya kimuqawama ya Wapalestina katika ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan iliyopelekea kujeruhiwa wanajeshi saba wa Israel na kueleza kwamba, jinai za Israel zinazidi kuimarisha irada ya muqawama wa Wapalestina.

Tariq Izzuddin, msemaji wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amebainisha kuwa, operesheni ya al-Khalil inathibitisha kuendelea muqawama dhidi ya utawala vamizi wa Israel unaotenda jinai kila uchao huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kiongozi huo wa Harakati ya Jihadul-Islami ameongeza kuwa, kile kinachoshuhudiwa  hivi sasa huko al-Khalil ni muendelezo wa muqawama wa kishujaa wa Wapalestina.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilisisitiza kuwa, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Jenin vimekuwa hifadhi na nguzo ya muqawama.

Vijana na makundi ya muqawama ya Palestina yametangaza mara kadhaa kuwa, mapambano baina yao na utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu yako wazi kote Palestina na ni mapambano ya pande zote.

Inaelezwa kuwa, muqawama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umepiga hatua kwa kumiliki silaha sambamba na kutekelezwa operesheni za kutumia silaha baridi na kuwadhibiti Wazayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *