Jumuiya ya Kitaifa na Kiislamu nchini Bahrain ya Al-Wifaq imetangaza kuwa, uchaguzi ujao wa Bunge nchini humo ni wenzo na chombo cha kuimarisha dhulma na kuendelea ufisadi
Hayo yameelezwa na Sheikh Hussein al-Daihi, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa na Kiislamu nchini Bahrain ya Al-Wifaq ambaye amesisitiza kuwa, ”kubakia mgogoro wa kisiasa na hali ya sasa ya nchi hiyo” ni katika misingi isiyotetereka ya utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa.
Ameongeza kuwa, huu ni ukweli ambao unamdhihirikia kila mweledi wa masuala ya kisiasa ya Bahrain na kwamba, utawala wa Manama unapaswa kuhitimisha kutumia mkono wa chuma na ukandamizaji sambamba na kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa.
Uchaguzi wa Bunge nchini Bahrain umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Hata hivyo mrengo wa upinzani nchini humo umetangaza kususia uchaguzi huo.
Tangu ulipoanza ukandamizaji dhiidi ya vuguvugu la mapambano ya wananchi lililoanza mwaka Februari 14, 2011 hadi sasa, Bahrain imeendelea kushuhudia wimbi kubwa la malalamiko na upinzani wa umma unaotaka marekebisho ya kisiasa yafanyike nchini humo.
Katika kipindi chote hiki kunashuhudiwa makabiliano baina ya wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa na wananchi. Katika hali ambayo, utawala wa Aal Khalifa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita, haujaheshimu haki yoyote ile ya wananchi wa nchi hiyo iwe ya kisiasa au ya kiraia, hivi sasa unataka kufanyike uchaguzi mpya wa Bunge ili ujionyesha kwamba, unazingatia masuuala ya demokrasia.