Wafanyaziara milioni 24 washiriki matembezi Arbaeen ya Imam Hussein AS huko Karbala, Iraq

Wafanyaziara milioni 24 wamekusanyika katika mji wa Karbala wa Iraq kuadhimisha Arbaeen, tukio la kila mwaka ambalo linaadhimisha siku ya 40 baada ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa madhehebu ya Shia.

Mjumuiko wa Arbaeen huko Karbala Iraq, umetajwa kuwa mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini ulimwenguni, unaowaleta pamoja mamilioni ya wafanyaziara kutoka Iraq na Iran na pia mataifa mengine duniani.

Wafanyaziara ambao aghalabu walivalia mavazi meusi kama ishara ya maombolezo walikusanyika katika haram tukufu ya Imam Hussein AS huko Karbala siku ya Jumamosi katika kilele cha matembezi ya zaidi ya wiki moja ya ukumbusho wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Mohammad (SAW), ambaye aliuawa shahidi pamoja na masahaba zake wakati wa vita vya Karbala mwaka 61 Hijria Qamaria au 680 Miladia.

Wanaume, wanawake, vijana na wazee walikusanyika kwa mamilioni katika mji huo wa Iraq ili kutoa heshima zao kwa Imam Hussein (AS), ambaye ni kiongozi na mbeba bendera ya vita dhidi ya dhulma na ukandamizaji.

Tukio hilo la kila mwaka, ambalo ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani, huleta pamoja umati wa wapenzi na waumini wa Imam Hussein AS kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya matembezi ya kilomita 80 kati ya miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.

Mahema na stendi maalumu zinazoitwa Moukeb kwa Kiarabu huwekwa kwenye njia inayoelekea kwenye Haram ya Imam Hussein ili kuwapa mahujaji chakula na huduma nyinginezo.

Katika miaka miwili iliyopita, makadirio ya mahudhurio yalikuwa chini kuliko kawaida kwa sababu ya janga la corona ambalo lilipunguza idadi ya mahujaji wa kigeni wanaoingia Iraq.

Kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita, wafanyaziara kutoka nchi kadhaa zikiwemo Iran, Afghanistan, Pakistan, Jamhuri Azerbaijan, Bahrain, Kuwait na Saudi Arabia wamekuwa wakiwasili Karbala, iliyoko takriban kilomita 100 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Serikali ya Iran ilisema Jumatano kwamba wafanyaziara wa Iran zaidi ya milioni tatu, walimiminika Iraq kushiriki katika kumbukumbu za Arbaeen.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *