Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, Muqawama ndio njia pekee ya kukabiliana na adui mzayuni. Nasrullah ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa siku ya Jumamosi kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein AS.
Kwa hivyo, moja ya sababu za kuendelezwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na hata Walebanon ni kwamba, kwa upande mmoja, utawala huo wa Kizayuni haukuadhibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote kwa kufanya jinai hiyo ya kutisha zaidi; na kwa upande mwingine, wahaini na wasaliti wa ndani ya Lebanon, nao pia si tu hawakuadhibiwa kwa kushirikiana na utawala huo, lakini wangali wako kwenye ulingo wa siasa za Lebanon wakiungwa mkono wa Wazayuni na waungaji mkono wao wa Magharibi. Na ndio kusema kuwa, maadamu hiyo ndio hali inayoendelea kutawala, jinai za utawala wa Kizayuni hazitakomeshwa, wala nchi kama Lebanon haitaweza kuwa na uthabiti wa kisiasa na kiusalama.
Kimsingi ni kwamba, siasa na sera za Marekani ndio sababu kuu ya kuendelea jinai za Wazayuni, hususan dhidi ya Wapalestina. Muamala wa Karne, ambao ulibuniwa na kutekelezwa na serikali iliyopita ya Marekani ni miongoni mwa sera iliyoonyesha wazi kuwa lengo lake lilikuwa ni kukidhi maslahi ya utawala huo ghasibu na kukandamiza maslahi ya Wapalestina; na ukachochea zaidi kushadidishwa ukatili na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Baada ya kutekelezwa mpango huo wa kibaguzi wa Muamala wa Karne, utawala wa Kizayuni umeweza kuendeleza kwa wepesi zaidi na bila ya hofu yoyote mipango na njama zake dhidi ya Wapalestina.