Sheikh Zakzaky: Saudia ilihusika katika mauaji ya wafuasi wa Ahlul Bait (AS) huko Zaria

Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, Saudi Arabia ilikuwa na nafasi katika mauaji ya wafuasi wa Ahlul Bait (as) katika mji wa Zaria mwaka 2015 yaliyotekelezwa na jeshi la Nigeria.

Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema katika mahojiano maalumu na televisheni ya Al-Alam, ambayo maelezo yake yatatangazwa baadaye, kwamba mauaji ya Zaria yaliyofanywa na maafisa wa serikali ya Nigeria mwaka 2015 dhidi ya wafuasi wa Ahlul-Bait (as) yalitekelezwa kwa amri ya Washington na London na kwamba Riyadh pia ilishiriki katika mauaji hayo.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia amesisitiza kuwa harakati hiyo inafuatilia kesi hiyo kupitia malalamiko yaliyowasilishwa na Jumuiya ya Haki za Waislamu ya London katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Matukio ya Zaria yanahusu mauaji ya zaidi ya watu elfu mbili na kujeruhiwa kwa idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mwishoni mwa mwezi wa Safar, Disemba 12 na 13, 2015, ambayo yalitekelezwa kwa shambulio la Jeshi la Nigeria dhidi ya Husainiya ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria, kitovu cha wafuasi wa Ahlul Bait nchini Nigeria na makazi ya kiongozi wao.

Katika tukio hili, Sheikh Zakzaky na mkewe walijeruhiwa na kutiwa mbaroni, na Ali, mmoja wa watoto wa Sheikh Zakzaky, pamoja na rafiki yake wa karibu ambaye pia alikuwa naibu wake, Sheikh Mohammad Mahmoud Turi na maafisa wengine kadhaa wa  wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, walikuwa miongoni mwa Waislamu elfu mbili aliouawa shahidi katika hujuma hiyo.

Askari walioshambulia Husainiya ya Baqiyyatullah waliwafungia Waislamu waliokamatwa kwenye chumba na kuwachoma moto wakiwa hai. Kutokana na shambulio hilo pia, takriban watu mia nane walitoweka na hadi sasa hatima yao haijulikani.

Baada ya mauaji hayo, watu wa Nigeria walianza maandamano makubwa ambayo bado yanaendelea, na maafisa wa serikali hawajaweza kuzima moto huo ambao uliwashwa na hatua za jeshi mnamo 2015, licha ya ukandamizaji mkubwa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *