Utawala wa Kizayuni wakasirishwa na Australia kubadilisha msimamo wake kuhusu Baitul Muqaddas

Viongozi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamesema wamekasirishwa na hatua ya serikali mpya ya Australia ya kufuta uamuzi wa serikali iliyopita wa kuitambua Baitul Muqaddas (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala huo ghasibu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong alitangaza Jumanne kwamba serikali ya Australia itafuta uamuzi wa baraza la mawaziri lililopita wa kuitambua Baitul Muqaddas kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA ikilinukuu gazeti la Kizayuni la Israel News, waziri ,kuu wa Israel Yair Lapid alisema jana hiyohiyo kuhusu hatua ya chama tawala cha Australia ya kubadilisha msimamo wa awali wa nchi hiyo kuhusu kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala huo kwamba, kubadilika msimamo wa serikali mpya ya Australia kunatia wasiwasi.
Lapid amedai kuwa hatua ya Chama cha Leba nchini Australia, ambacho sasa ndicho chama tawala cha nchi hiyo, imetegemea ripoti isiyo sahihi ya vyombo vya habari na ni “hatua ya pupa” na akaongezea kwa kusema: “Tunatumai kwamba serikali ya Australia itakuwa na umakini zaidi katika masuala mengine.”

Katika taarifa iliyotolewa jana, wizara ya mambo ya nje ya utawala wa Kizayuni ilitangaza kuwa, imemwita balozi wa Australia kulalamikia suala hilo na kubainisha kuwa: Israel inaonyesha masikitiko yake makubwa juu ya uamuzi huo wa serikali ya Australia ambao imedai umezingatia sababu zenye uono mdogo wa kisiasa.

Moshe Leon, meya mzayuni wa mji wa Baitul Muqaddas, ameonyesha kughadhibishwa na uamuzi na Australia na kuelezea kwamba hatua hiyo ya Canberra haina faida yoyote kwa ajili ya kupatikana haki za Wapalestina.
Itakumbukwa kuwa Scott Morrison, waziri mkuu wa zamani wa Australia, alitangaza mwaka 2018 kwamba anafikiria kuitambua Quds inayokaliwa kwa mabavu kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na ikiwezekana kuuhamishia ubalozi wa Australia ulioko Tel Aviv kwenye mji huo.
Hatua hiyo ya Morrison ilikosolewa vikali na makundi ya Wapalestina pamoja na chama cha Leba cha Australia ambacho wakati huo kilikuwa chama kikuu cha upinzani na kuahidi kuubadilisha uamuzi huo kitakapochaguliwa kuongoza serikali.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *