Kaburi la umati lenye miili 25 laguduliwa kaskazini mwa Malawi

Malawi imetangaza kuwa, imegundua kaburi la umati kaskazini mwa nchi hiyo lenye mabaki ya watu 25 wanaoshukiwa kuwa wahamiaji kutoka Ethiopia.

Taarifa iliyotolewa na polisi ya Malawi imeeleza kuwa, “kaburi hilo liligunduliwa Jumanne jioni, lakini tulilizingira na kuanza kufukua jana. Kufikia sasa, tumegundua miili 25. Hayo yameelezwa na  msemaji wa polisi ya Malawi Peter Kalaya alipozungumza na duru za habari.

Polisi walitahadharishwa na wanakijiji katika eneo la Mzimba, yapata kilomita 250 kaskazini mwa mji mkuu, Lilongwe, ambao waliona kaburi hilo wakati wakikusanya asali mwitu msituni.

Msemaji wa polisi ya Malawi ameongeza kuwa: Tunashuku kuwa walikuwa wahamiaji haramu ambao walikuwa wakisafirishwa hadi Afrika Kusini kupitia Malawi.

Aidha amesema kuwa, ushahidi uliokusanywa kutoka kwenye eneo hilo ulionyesha waathirika walikuwa wanaume raia wa Ethiopia wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 40.

Miili hiyo iliyoharibika ilitolewa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, miili hiyo ilizikwa katika kaburi la umati si zaidi ya mwezi mwezi.

Malawi ni njia maarufu kwa watu kutoka Afrika Mashariki wanaosafirishwa hadi Afrika Kusini – nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda katika bara hilo na kivutio cha wahamiaji maskini kutoka mahali pengine barani.

Kalaya alisema kuwa kati ya Januari na Septemba mwaka huu, mamlaka ilikamata wahamiaji 221, 186 kati yao wakiwa Waethiopia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *