FAO : Zaidi ya watu milioni 4 wameathiriwa vibaya na ukame nchini Kenya

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni 4 wameathiriwa vibaya na ukame nchini Kenya.

Maelfu ya watoto wanahangaika kupata lishe huku baadhi ya wanafunzi wakilazimika kuacha shule kutokana na makali ya njaa yanayozikabili familia zao.

Ripoti ya FAO inaeleza kuwa, katika Kaunti za kaskazini mashariki mwa Kenya athari ya ukame inazidi kuleta maafa makubwa huku watoto wadogo wakipata utapia mlo.

Hali hii huenda ikawa mbaya zaidi iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa huku waathiriwa wakuu wa ukame na njaa wakiwa ni wanawake na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Mwaka huu sehemu kame zilipokea mvua kwa kiwango cha chini Zaidi kuwahi kushuhudiwa na kuathiri sana uzalishaji wa mimea na vyakula vya mifugo.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, kwa misimu minne iliyopita ya mvua, mvua za kila mwaka hazikunyesha kote nchini Kenya, Ethiopia na Somalia na kuwalazimu watu milioni 1.5 kukimbia makazi yao kutafuta chakula na maji kwingineko.

Wakati huo huo, shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children linakadiria kwamba, takriban watoto milioni mbili katika Pembe ya Afrika wanahitaji matibabu ya haraka kwa utapiamlo unaotishia maisha yao.

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema, watoto milioni 3.6 huko Kenya, Somalia na Ethiopia wako katika hatari ya kuacha shule katika misimi minne mtawalia ya ukame na hivyo kuzilemea familia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *