Duru za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel zimeripoti kuwa, safari zisizopungua 10 za ndege za utawala huo haramu kuelekea India zimefutwa baada ya Oman kukataa kuzipatia ndege hizo kibali cha kupita katika anga yake.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Shahab News, ripota wa redio ya jeshi la utawala wa Kizayuni amethibitisha habari hiyo na kueleza kwamba, zaidi ya safari kumi za ndege zinazotoka Israel kuelekea India zimefutwa; na sababu ni kuwa viongozi wa Oman wamekataa kutoa kibali kwa mashirika ya ndege ya utawala huo wa Kizayuni kutumia anga ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo msimamo huo wa kila mara wa Oman umeyasababishia hasara kubwa mashirika hayo ya ndege kutokana na kulazimika kufuta safari zao na kuwarejeshea abiria nauli zao.
Kabla ya hapo, Saudi Arabia iliruhusu anga yake kutumiwa na ndege za mashirika ya ndege ya Israel zinazoelekea India, lakini makubaliano ya Riyadh na Tel Aviv hayakuweza kufanya kazi kutokana na kukataa Oman kutoa kibali cha kutumiwa anga yake na ndege hizo.
Japokuwa utawala wa Riyadh ulitoa idhini ya kutumiwa anga yake na ndege za mashirika ya ndege ya utawala wa Kizayuni zinazofanya safari zao kuelekea India, lakini ndege hizo zinahitaji kutumia anga ya Oman pia ili kufupisha masafa ya safari hizo kuelekea mashariki ya Asia.
Hatua ya Oman imefelisha mapatano hayo yaliyokuwa yamefikiwa kati ya Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel, ambayo yalitokana na uamuzi uliotangazwa na Riyadh mwezi Juni mwaka huu kwamba inafungua anga yake ili kutumiwa na mashirika yote ya ndege duniani.