Maelfu waandamana nchini Ethiopia kupinga uingiliaji wa Marekani nchini humo

Maelfu ya Waethiopia walifanya maandamano ya nchi nzima siku ya Jumamosi kulaani kile walichokitaja kama uingiliaji wa madola ya kigeni, hasa Marekani, katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Katika mji mkuu Addis Ababa, waandamanaji walibeba mabango yaliyosomeka “Tishio kwa Ethiopia ni tishio kwa ulimwengu” na “heshimu uhuru wa kujitawala Ethiopia.” Mabango mengine yalikuwa na maneno ya kuishutumu Marekani kwa kutoheshimu uhuru wa Ethiopia.

Akizungumza mbele ya umati mkubwa , Jantrar Abay, naibu meya wa Addis Ababa alisema, “Nchi za kigeni zinapaswa kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Ethiopia na zinapaswa kuacha kuunga mkono vikosi vya waasi, haswa kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF) na washirika wake,”

“Utawala wa Ethiopia lazima uheshimiwe, Waethiopia wataendelea kusimama kwa umoja ili kulinda uhuru wa nchi yao”, aliongeza.

Maandamano hayo pia yalifanyika katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Maandamano hayo yalikuja huku serikali ya Ethiopia ikiwa chini ya mashinikizo kufuatia kuanza tena mapigano mwezi Agosti kaskazini mwa Ethiopia kati ya vikosi vya serikali na waasi wa TPLF baada ya kusitisha mapigano kwa muda wa miezi mitano.

Serikali ya Ethiopia ilishutumu TPLF kwa kuanzisha tena mapigano ya hivi karibuni ambayo yalisimamisha ufikishaji  misaada ya kibinadamu katika maeneo ya kaskazini mwa Ethiopia.

Mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi yanatarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini wiki ijayo.

Demeke Mekonnen, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, aliwaambia wanadiplomasia nchini humo siku ya Jumamosi kwamba,”Ethiopia iko tayari kwa mazungumzo ya amani yatakayofanyika Afrika Kusini, kwani serikali imekuwa ikisema iko tayari kwenda popote na wakati wowote kutatua mzozo huo kwa amani,”

Aidha amesema TPLF lazima inyimwe fursa ya kujiimarisha na kuhamasishana tena kwa awamu ya nne ya mzozo.

Siku ya Jumanne, serikali ilitangaza mipango ya kurejesha misaada na huduma za kibinadamu katika maeneo ambayo jeshi limeyakomboa kutoka udhibiti wa waasi wa TPLF.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *