Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kampuni kubwa ya saruji ya Ufaransa ya Lafarge sasa imefichuliwa kuwa moja ya taasisi muhimu zinazounga mkono ugaidi.
Akizungumza katika Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa Habari wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ulioanza Ijumaa na kumalizika jana mjini Istanbul, Erdogan ameongeza kuwa, “Niliposema jinsi kampuni kubwa ya saruji ya Ufaransa, inayoitwa Lafarge, ilivyosaidia na kuunga mkono makundi ya kigaidi kaskazini mwa Syria, Wafaransa hawakuelewa hili.
Nilimfahamisha hayo (Rais wa Ufaransa Emmanuel) Macron. Sasa katika bunge la Ufaransa, wamemtaka Macron atoe ufafanuzi kuhusu Lafarge.”
Erdogan ameongeza kuwa, “Kwa sasa, Lafarge imekuwa moja ya masuala muhimu katika ajenda ya Ufaransa. Lafarge sasa imefichuliwa kikamilifu kama moja ya taasisi muhimu zinazounga mkono ugaidi.”.
Lafarge alipigwa faini kubwa ya dola milioni 778 Jumanne kwa kuunga mkono makundi kadhaa ya kigaidi nchini Syria mwaka 2013-2014, ikiwa ni pamoja na kundi la Daesh/ISIS.
Erdogan ameendelea kusema kwamba wale walioituhumu Uturuki “walifanya biashara na Deash, wakafanya biashara na kuhamisha mamilioni ya euro kwa magaidi katika kipindi hicho.’.
Kwingineko katika hotuba yake, Erdogan ameuambia mkutano huo kuwa mseto wa vyanzo vya habari na kuongezeka kwa ushiriki wa vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii, katika maisha ya kila siku huleta faida nyingi pamoja na hatari kubwa.
Amefafanua kwa kusema kuwa, uchafuzi wa kihabari na habari potofu ni sehemu kuu ya hatari hiyo.
Katika mkutano huo wa siku mbili, mawaziri na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka nchi 57 wanachama wa OIC wamejadili masuala yatakayoimarisha ushirikiano katika nyanja za vyombo vya habari, mawasiliano na habari katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mkutano huo uliofanyika chini ya kaulimbiu ya Kupambana na Taarifa Potofu na Chuki dhidi ya Uislamu, umelenga kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Kiislamu katika uga wa vyombo vya habari na mawasiliano.
Rais Erdogan amesema habari za uongo na usaidizi kwa mashirika ya kigaidi ni upande mmoja wa sarafu, na pande mwingine ni chuki dhidi ya Uislamu na wageni.