Leo wananchi wa Iran wanafanya maadamano ya nchi nzima kulaani shambulio la kigaidi

Wananchi wa jiji la Tehran na miji yote ya Iran, leo baada ya Sala za Ijumaa, watafanya maandamano makubwa ya nchi nzima kulaani shambulio la kigaidi lililotokea juzi Jumatano katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh ya mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran. Genge la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na jinai hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, maandamano hayo ya leo mchana ya baada ya Sala za Ijumaa, yatafanyika kwa wakati mmoja na kushirikisha watu wa kada zote wa kona zote za Iran.

Kufuatia tukio la kigaidi lililotokea katika Haram ya Ahmad bin Musa (Shah Cheragh) huko Shiraz, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa akisisitiza kuwa wahalifu waliohusika na jinai hiyo wataadhibiwa.

Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, watu wasiopungua 15 wameuawa huku 27 wakijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la juzi Jumatano yapata saa 12 kasorobo jioni kwa majira ya hapa Iran katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, katika mkoa wa Fars wa kusini magharibi mwa Iran.

Hadi hivi sasa nchi mbalimbali duniani zimeshatoa mkono wao wa pole kufuatia shambulio hilo la kigaidi. Miongoni mwa nchi hizo ni Russia, China, Uturuki, Pakistan, Armenia, Jamhuri ya Azerbaijan, Misri, Imarati, Venezuela, Oman, Syria, Iraq, Finland, Umoja wa Mataifa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Kataib Hizbullah ya Iraq, Ansarullah ya Yemen n.k, zimetoa mkono wa rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kufuatia jinai hiyo iliyofanywa na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, (ISIS).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: “Sisi sote tuna wajibu wa kumshughulikia adui anayewasha moto wa fitina na vibaraka wake, wasaliti na wajinga na walioghafilika.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *