Mashirika ya kijasusi ya kigeni yakiongozwa na CIA yamehusika na ghasia Iran

Taarifa ya pamoja ya Wizara ya Intelijensia ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imesema mashirika ajinabi ya kijasusi yakiongozwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) yamekuwa na mchango mkubwa katika kupanga na kuratibu ghasia na fujo zilizoshuhudiwa hapa nchini kwa wiki kadhaa.

Taarifa hiyo imesema CIA ya Marekani ilikuwa imepanga mkakati mpana kwa ushirikiano na taasisi za kijasusi za waitifaki wa Washington wa kuvuruga usalama wa Iran, kufanya jinai dhidi ya Wairani na kukiuka mamlaka ya kujitawala taifa hili, hata kabla ya kuaga dunia Mahsa Amini.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Marekani ilitanga bajeti ya dola milioni 53 na kuyapa mashirika hayo ajinabi ya kijasusi ili kutekeleza amri na njama za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) hapa nchini.

Taarifa ya pamoja ya Wizara ya Intelijensia ya Iran na Jeshi la SEPAH imefichua kuwa, mashirika hayo ya kijasusi yanafanyakazi bega kwa bega na utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya ili kujaribu kutekeleza njama hizo ghalati, ambazo hata hivyo zimegonga mwamba.

Imesema maadui wa taifa hili wamepanga njia mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza ‘vita vya vyombo vya habari’ dhidi ya Iran, kupitia televisheni, tovuti za habari na mitandao ya kijamii.

Taarifa hiyo imefichua kuwa, baina ya Septemba 11 na Oktoba 12, mtandao wa kijamii wa Twitter uliruhusu kufunguliwa akaunti  feki 50,000 za lugha ya Kifarsi, zinazotumiwa kueneza propaganda na kusukuma mbele ajenda za maadui dhidi ya Iran.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema karibuni hivi itawawekea vikwazo shakhsia na taasisi za Marekani na Canada kwa ungaji mkono wao kwa vitendo vya kigaidi na machafuko ya ghasia hapa nchini.

Msemaji wa wizara hiyo, Nasser Kan’ani amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hatua ya kujibu mapigo, itaziwekea vikwazo taasisi na shakhsia kadhaa wa Marekani na Canada kwa sababu ya vitendo vya makusudi vya kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi, kueneza na kuchochea ugaidi na machafuko, kueneza chuki zilizosababisha uvurugaji amani na kuzusha ghasia, kuchukua hatua za kigaidi na kukiuka haki za binadamu za wananchi wa Iran.

Hivi karibuni, Iran iliziwekea vikwazo pia taasisi na shakhsia kadhaa wa Umoja wa Ulaya kutokana na hatua zao za makusudi za kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi, mbali na kuwasha moto wa ghasia hapa nchini.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *