Maandamano Uingereza kulaani polisi wanaowaua watu wenye asili ya Afrika

Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Uingereza, London, kupinga ubaguzi wa rangi ulivyokita mizizi katika jeshi la polisi nchini humo.

Waandamanaji waliokuwa na hasira walifika katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ili kuufahamisha umma kuhusu visa vya kutisha vya namna ambavyo, vijana ambao aghalabu wana asili ya Afrika wanavyopoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha wakiwa mikononi mwa polisi.

Familia za waathirika na waungaji mkono wao hukutana kila baada ya miaka miwili mwishoni mwa mwzi wa Oktoba kulaani ukatili huo wa jeshi la polisi nchini Uingereza. Maandamano hayo yamekuja wakati bado watu wanakumbuka mauaji ya hivi karibuni ya kijana mwenye asili ya Afrika, Chris Kaba, ambaye alipigwa risasi na kuuawa na polisi eneo la London Kusini katika hali ambayo hakuwa na silaha yoyote.

Chris Kaba alipigwa risasa na kuuawa na afisa wa polisi Septemba tano na mauaji hayo yaliibua hasira kubwa ambapo yamelinganishwa na mauaji ya George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyeuawa kinyama na polisi nchini Marekani Mei 2020.

Maandamano hayo ya London yameandaliwa na Muungano wa Familia na Marafiki wa Waliouawa (UFFC) mikononi mwa polisi watenda jinai Uingereza. Muungano huo sasa unajumuisha familia za watu wa rangi zote ambao jamaa zao wamefariki wakiwa mikononi mwa polisi nchini Uingereza.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *