Kusambazwa picha za tamasha la kishetani la “Halloween” katika mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh kwa usaidizi na uungaji mkono wa Bodi ya Burudani ya nchi hiyo kumeibua wimbi la hasira kali na kauli za kejeli kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Falastin al-Yaum, watumiaji wa mitandao ya kijamii wameandika kuhusu tamasha la kishetani la Halloween lililofanyika mjini Riyadh kwamba, Wamagharibi hujiburudisha kwa kufanya matamasha ya aina hiyo, lakini kwa nchi ya Waislamu ni hatari kusherehekea jambo hilo kwa sababu nchi za Kiislamu zina mila na desturi zao za Kiislamu.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wameeleza pia kuwa tamasha la Halloween lililofanyika mjini Riyadh ulikuwa ni uvunjaji miiko mbaya zaidi ambao umefanywa na Bodi ya Burudani ya utawala wa Aal Saud.
Mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “tatizo kubwa zaidi ni kwamba, hatua hii imechukuliwa kwa uungaji mkono rasmi na hakuna yeyote miongoni mwa maulamaa na wananchi awezaye kukemea na kulaani, kwa sababu endapo watathubutu kufanya hivyo haijulikani watafikwa na hatima gani”.
Inafaa kuashiria kuwa, maelfu ya watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wamekemea hatua hiyo na uigaji kibubusa wa mila za Magharibi na wakaeleza kwamba, “kwa miaka mingi ilikuwa marufuku nchini Saudi Arabia kufanya sherehe na matamasha ya aina hiyo, lakini mwaka huu tunawaona watu wanazunguka mitaani na mavazi ya ajabu ajabu”.