Rekodi mbaya ya mmiliki mpya wa Twitter, Elon Musk ya kuchukua misimamo isiyo ya kawaida na kuibua masuala yenye utata imeufanya Umoja wa Mataifa kumuonya dhidi ya kuchapisha maudhui yoyote ya chuki katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Ripoti ya shirika la habari la Sputnik imemnukuu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akisema: “Tumetangaza kwa wasiwasi kwamba Twitter na mitandao mingine ya kijamii haipaswi kutumiwa kueneza chuki, maudhui yasiyo ya kweli au ubaguzi wa rangi, kwa sababu hiyo tunafuatilia suala hili kwa karibu.”
Ukurasa wa Umoja wa Mataifa kwenye mtandao wa Twitter wenye wafuasi na watumiaji milioni 16 ni mojawapo ya kurasa zinazotumika sana za mtandao huo wa kijamii, na maafisa wote, idara na ofisi za shirika hilo zina akaunti kwenye Twitter.
Mara baada ya kukamilika kwa makubaliano ya ununuzi wa Twitter, Elon Musk alianza kutimua idadi kubwa ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, suala ambalo limeibua wasiwasi kuhusu sera mpya la mtandao huo. Siku chache zilizopita, gazeti la Marekani la Washington Post lilinukuu nyaraka za Twitter na kuandika kwamba mmiliki mpya wa kampuni hiyo, Elon Musk anapanga kufuta kazi asilimia 75 ya wafanyakazi wa Twitter.
Hivi karibuni pia Wizara ya Usalama wa Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirika la Upepelezi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilitoa taarifa ya pamoja zikiashiria hatua za kueneza chuki na uchochezi za mtandao wa kijamii wa Twitter na kuondoa mipaka na masharti kwa watumiaji wake kwa kuwaruhusu kuchapisha maudhui za kichochezi, uongo na chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.