Polisi ya Afrika Kusini inachunguza kisa cha kugunduliwa makumi ya maiti za watu wanaoshukiwa kuwa wachimba migodi ‘haramu’ katika mji wa Krugersdorp, magharibi mwa jiji la Johannesburg.
Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini, Brenda Muridili amesema waliopoa maiti 19 kwenye mgodi binafsi katika mji huo hapo jana, huku miili mingine miwili ikigunguliwa mapema leo Alkhamisi.
Jeshi la Polisi nchini humo limesema yumkini wachimba migodi hao waliuawa sehemu tofauti, kisha miili yao ikapelekwa karibu na mgodi huo binafsi mjini Krugersdorp.
Kesi hiyo ni sehemu ya wimbi la matukio ya kihalifu yanayohusishwa na uchimbaji madini kinyume cha sheria katika mji wa Krugersdorp, ulioko magharibi mwa mji wa Johannesburg ambao ni makao makuu ya mkoa wa Gauteng.
Julai mwaka huu, wanawake wanane waliokuwa katika timu ya kutengeneza filamu walibakwa na mali zao kuporwa katika mgodi uliotelekezwa eneo la Krugersdorp.
Kutokana na hali ngumu ya maisha, akthari ya wananchi wa Afrika Kusini katika maeneo yenye utajiri wa madini wamekuwa wakichimba migodi ambayo sio salama, kinyume cha sheria.
Hata hivyo wadadisi wa mambo wanavilaumu vyombo vya dola nchini humo, kwa kushindwa kudhibiti shughuli hizo za uchimbaji madini kinyume cha sheria.