Ndege ya abiria yaanguka Tanzania; watu 19 wathibitishwa kuaga dunia

Kwa akali watu 19 wameaga dunia nchini Tanzania, baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air kuanguka katika Ziwa Victoria jiirani kabisa na uwanja wa ndege wa Bukoba.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila idadi ya waliofariki imefikia 19, majeruhi 26.

Ndege ya Shirika la Ndege ya Precision Air ilipata ajali mapema leo na kutumbukia Ziwa Viktoria huko nchini Tanzania, mita 100 kabla ya kutua Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa  taarifa ndege ya Precision Air namba PW494 ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba,

Ilianguka katika Ziwa Victoria leo asubuhi, muda mfupi kabla ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema watu 19 wamethibitishwa kufariki dunia na kuna watu 26 waliojeruhiwa mbao ni manusura wa ajali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Bukoba, Chalamila amesema ndege hiyo ilikuwa na jumla ya watu 43 ambapo kati yao 39 ni abiria, wahudumu wawili na marubani wawili.

Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha sehemu ya ndege hiyo iliyozama ikiwa imezungukwa na boti za uokoaji.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kutokana na mkasa huo.

Katika ujumbe wake, Rais Samia amesema: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera. Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii. Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *