Wauguzi wa Uingereza wamepiga kura kwa mara ya kwanza kugoma kitaifa kiviwanda kabla ya Krismasi, kwani kuongezeka kwa kiwango cha mfumuko wa bei kumewaingiza Waingereza wengi katika hali mbaya ya kiuchumi.
Maafisa wa vyama vya wafanyakazi wanasema wauguzi katika “maeneo mengi ya ya nchi” wanaofanya kazi katika majimbo ya England, Scotland, Wales na Ireland Kaskazini walipiga kura ya kugoma baada ya wanachama 300,000 kuuunga mkono hatua hiyo.
Jumuiya hiyo ya wauguzi, RCN, inatazamiwa kufichua matokeo ya mwisho ya kura yake, katika siku chache zijazo huku zoezi kuhesabu kura kukiendelea.
Jumuiya hiyo ya wauguzi imesema wanachama wake wamekabiliwa na muongo mmoja wa kupunguzwa mishahara, na inafanya kampeni ya nyongeza ya mishahara ya asilimia tano juu ya mfumuko wa bei unaoongezeka ambao unafikia rekodi ya juu ya asilimia kumi.
“Hatua yetu ya mgomo itakuwa kwa maslahi ya wagonjwa kama ilivyo kwa wauguzi – tuna uungaji mkono wao (wagonjwa) katika kufanya hivi,” Pat Cullen, katibu mkuu wa RCN, alisema katika taarifa.
“Idadi kubwa ya wafanyakazi – waajiriwa wenye uzoefu na wapya – wanaamua kuwa hawakubali kuona mustakbali wa taaluma ya uuguzi ambayo haithaminiwi au kutendewa haki.”
Ingawa watu milioni 7 ambao wanasubiri matibabu katika hospitali nchini Uingereza sasa wana uwezekano wa kuona matibabau yao yakicheleweshwa au kughairiwa, wauguzi katika vitengo vya wagonjwa mahututi na vitengo vya dharura na ajali (A&E) hawataruhusiwa kushiriki.
Uchambuzi wa Nuffield Trust uliochapishwa mapema mwaka huu uliripoti kuwa muuguzi mmoja kati ya tisa alikuwa ameacha Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza (NHS) kufikia Juni 2022, ikiashiria zaidi ya nafasi 46,000 za uuguzi katika NHS eneo la England pekee.
Makumi ya maelfu ya wafanyakazi katika tasnia mbali mbali, wafanyakazi wa reli na posta pia wamegoma kote Uingereza tangu msimu wa joto, kwani shida ya gharama ya maisha imewasukuma wafanyakazi kuondoka na kudai nyongeza ya mishahara sambamba na mfumuko wa bei.