Jordan yaonya kuhusu hatua za Israel za kuzusha mizozo Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan ameonya kuhusiana na hatua za utawala haramu za Israel za kuzusha mivutano na mifarakano dhidi ya Wapalestina.

Ayman Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan amesema hayo katika mazungumzo yake na mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mwenendo wa amani ya Asia Magharibi na kutahadharisha kuhusiana na hatari ya kushadidi hatua za uchochezi na kuzusha mivutano dhidi ya Wapalestina zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan amesisitiza pia juu ya udharura wa kuheshimiwa hali ya kihistoria na kisheria iliyopo katika maeneo matukufu ya Kiislamu na kihistoria huko Beitul-Muqaddas na kukomesha aina yoyote ile ya uchochezi, hujuma na uvamizi.

Hivi majuzi pia Ayman Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan sambamba na kusisitizia udharura wa kupatiwa ufumbuzi kadhia ya Palestina alitoa mwito wa kukomeshwa uvamizi, hujuma na mashambulio ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Istrael dhidi ya miji na vijiji vya Wapalestina.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *