Clopp: Acheni kuingiza siasa katika mashindano ya Kombe la Dunia Qatar 2022

Kocha mkuu wa timu ya soka ya Liverpool nchini Uingereza, Jurgen Klopp, amewakemea wale wanaowataka wachezaji wa kambumbu kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar kuchukua msimamo na kupinga masuala ya haki za binadamu na kutoa madai dhidi ya Qatar, akisema matakwa hayo yanapaswa kusitishwa.

Tangu Qatar iliposhinda mchuano wa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka hapo 2010, daima imekuwa chini ya mashinikizo ya nchi za Magharibi kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kutoheshimiwa haki za wafanyakazi wahamiaji wanaofanya kazi katika nchi hiyo.

Zikiwa zimebakia siku kadhaa kabla ya kuanza mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani, kocha mkuu wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp, amesema kuwa sasa ni wakati wa kuwaacha wachezaji na makocha waweke mazingatio yao kwenye soka na mpira wa miguu.

Awali Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino katika barua aliyoyaandikia mashirikisho ya soka ya nchi zinazoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Dunia Qatar 2022, aliyataka yazingatie soka pekee badala ya kuibua vita vya kiitikadi na kisiasa kwenye michuano huo.

Matamshi ya kocha wa Liverpool na barua ya Infantino yametolewa wakati Ukraine na baadhi ya nchi za Magharibi zikiitaka FIFA kuiondoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye mashindano ya Kombe la Dunia huko Qatar kwa madai ya uwongo kwamba Tehran imeiuzia Russia silaha na ndege zisizo na rubani.

Michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, ambayo itafanyika kwa mara ya kwanza katika eneo la Ghuba ya Uajemi katika msimu wa baridi, itaanza tarehe 20 mwezi huu wa Novemba na kuendelea hadi tarehe 18 Disemba.

Timu ya Taifa ya Iran (Tim-Melli) imepangwa katika kundi moja na nchi za Uingereza, Marekani na Wales.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *