Kanali ya televisheni ya KAN ya utawala wa Kizayuni, mapema leo Jumanne imetangaza habari ya kuangamizwa mlowezi mmoja Mzayuni anayejulikana kwa jina la Shalom Sofer ambaye alijeruhiwa katika operesheni moja ya mwanamapambano wa Palestina.
Televisheni hiyo imetangaza kuwa, Shalom Sofer alikuwa mlowezi wa Kizayuni anayeishi katika kitongoji cha Kedumim cha walowezi wa Kizayuni kilichojengwa kwenye ardhi walizoporwa Wapalestina baina ya Nablos na Qilqilya.
Mzayuni huyo alijeruhiwa kwenye operesheni ya muqawama wa Palestina huko Qilqilya wiki mbili zilizopita, na leo televisheni hiyo ya Kizayuni imetangaza kuwa ameangamia.
Tovuti ya “Quds al Ikhbariyyah” nayo imetangaza kuwa, mlowezi huyo wa Kizayuni alijeruhiwa vibaya katika operesheni ya wiki mbili zilizopita ya kujitolea kufa shahidi iliyofanywa na mwanamapambano wa Palesitna katika kijiji kimoja cha mashariki mwa Qilqilya.
Vyombo vya habari vya Kizayuni baadaye vilitangaza kuwa, wanajeshi wa Israel wamemkamata mwanamapambano huyo wa Palestina. Kwa kuuawa Mzayuni huyo kumeifanya idadi ya walowezi wa Kizayuni walioangamizwa katika opereseheni za muqawama wa Palestina tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kufikia 24.
Wakati huo huo wataalamu mbalimbali wametoa mwito kwa wananchi wa Palestina kujitokeza kwa wingi kuulinda Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu kilichoko chini ya njama chungu nzima na za kila upande za Wazayuni.
Msikiti wa al Aqsa ni nembo muhimu sana ya utambulisho wa Kiislamu – Kipalestina huko Baytul Muqaddas. Mwezi Oktoba 2017, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), lilitangaza kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni mali ya Waislamu na kwamba watu wengine hasa Mayahudi, hawahusiki kivyovyote vile na Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu.