Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wamemjibu Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia aliyedai kwamba hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kumueleza kuwa kutusi na kuvunjia heshima nchi ambayo ndani yake kuna Haram mbili za Makka na Madina haliwi suala la ndani la Saudia.
Ukurasa wa Twitter wa Nahwul-Hurriyah umeandika: “kuitusi na kuivunjia heshima nchi ya Haramaini si kadhia ya ndani-kuidunisha ardhi ya Mtume wa Allah si suala la ndani-kukivunjia heshima makusudi kibla cha Waislamu si suala la ndani”.
Jibu hilo limetolewa baada ya wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia kuripoti kauli iliyotolewa na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammed Bin Salman akisema, “hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuingilia masuala yetu ya ndani, kadhia hii inatuhusu sisi Wasaudia tu”.
Bin Salman ametoa kauli hiyo kufuatia kusambazwa hivi karibuni picha za tamasha la kishetani la “Halloween” katika mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh, ambalo lilifanyika kwa usaidizi na uungaji mkono wa Bodi ya Burudani ya nchi hiyo na kuibua wimbi kubwa la hasira na ukosoaji katika Ulimwengu wa Kiislamu.