Watu wenye silaha wateka nyara makumi ya watu Nigeria, 11 wauawa

Watu wenye silaha nchini Nigeria wamewateka nyara takriban watu 80 na kuwaua wengine 11 katika mashambulizi tofauti huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuwanukuu wakuu wa kimila na wakaazi wameneo hayo wakithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, katika mashambulizi ya hivi karibuni zaidi ya magenge yenye silaha ambayo yamekuwa yakivamia vijiji, ni yale yaliyotokea katika shule na barabara kuu.

Shirika la habari la Reuters aidha limeandika: Jimbo la Zamfara ni miongoni ya majimbo yaliyoathirika zaidi na magenge yenye silaha, yanayojulikana ndani ya Nigeria kwa jina la majambazi. Kazi yao kubwa ni kufanya ugaidi na kuwateka nyara watu ili wapate vikomboleo. Ukosefu wa usalama umeongezeka nchini Nigeria hivi sasa wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikikaribia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Februari 2023.

Taarifa nyingine imevinukuu vyombo vya habari vya kieneo nchini Nigeria vikisema kuwa, Gavana wa jimbo la Zamfara, Bello Matawalle na serikali yake ya jimbo hilo wamefanikisha kuachiliwa huru watu waliokuwa wametekwa nyara miezi sita iliyopita.

Hao ni miongoni mwa watu 23 waliotekwa nyara na majambazi wenye silaha katika Kijiji cha Furfuri kilichoko chini ya serikali ya mtaa wa Bungudu kwenye Jimbo la Zamfara mwezi Juni mwaka huu. Kijiji hicho kiko umbali wa kilomita 7 kutoka Gusau makao makuu ya jimbo la Zamfara.

Akiwapokea mateka hao kwenye Ikulu ya Serikali huko Gusau, Gavana Bello Matawalle amesema, watu hao wameokolowa kutokana na juhudi za Kamati ya Usalama ya Jimbo hilo baada ya wiki mbili za msako mkali msituni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *