Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump na washirika wake wa mrengo wa kulia katika chama cha upinzani cha Republican tayari wameanza kutilia shaka uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa Jumanne wa bunge wa katikati mwa muhula
“Haya twendeni tena! Uchaguzi wa hitilafu!,” CNN ilimnukuu Trump akiwaandikia wafuasi wake milioni 4.43 kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social ambapo aliambatanisha makala kwenye tovuti ya habari ya mrengo wa kulia ambayo iliibua shaka kuhusu utambulisho wa wapigakura ambao wanapiga kura kwa njia ya posta.
Makala hiyo iliyo katika tovuti ya kihafidhina ya Just The News inarejelea barua iliyotumwa kuhusiana na kadhia hii na wabunge 12 wa chama cha Republican kwa afisa wa umma wa Pennsylvania wakitaka ashughulikie kadhia ya vitambulisho.
Trump na washirika wake, ambao wanataka kushika usukani kwa mara nyingine, walikuwa wakifanya jitihada za muda mrefu mwaka 2020 kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo walisisitiza kuwa kulikuwa na wizi mkubwa wa kura uliopelekea Joe Biden apate ushindi. Wakati uchaguzi wa kati kati ya muhula wa Bunge la Kongresi la Marekani unafanyika leo Jumanne, baadhi ya Warepublican wa mrengo tayari wameshaanza kujitayarisha kupinga matokeo ya uchaguzi ikiwa chama chao kitashindwa.
Wakati huo huo, kulingana na ripoti, Wamarekani 9 kati ya 10 wanaogopa vurugu za kisiasa baada ya uchaguzi wa leo Jumanne.
Wafuasi wa chama tawala cha Democrat wanawalaumu Warepublican, nao Warepublican wanasema Wademokrat watabeba dhima iwapo ghasia zitaibuka huku kundi jingine la tatu la Wamarekani likisema vyama hivyo viwili vikubwa vinapaswa kulaumiwa iwapo vurugu za baada ya uchaguzi zitaibuka.
Ikumbukwe kuwa watu sita waliuawa katika ghasi za bada ya uchaguzi zilizoibuka katikak majengo ya Bunge la Kongresi mjini Washington D.C wakati wafuasi wa rais aliyeshindwa Donald Trump walivamia eneo hilo wakijaribu kuzuia wabunge kuidhinisha matokeo ya uchaguzi.
Kumekuwa na ongezeko la mara kumi la vitisho dhidi wabunge wa Kongresi kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuibuka tena kwa Trump, huku wafuasi wake wa mrengo wa kulia wakionekana kukandamizwa na kile alichokitaja kuwa “taifa la polisi” la chama tawala cha Democtrat kumefichua kuenea kwa kasi utamaduni hatari wa kisiasa wa wenye misimamo mikali wanaojiona wake kwenye haki mutlaki huku wakienza ghasia katika jamii.
Wakati huo huo, rais wa zamani Barack Obama, pamoja na Trump, kila mmoja ametahadharisha kuhusu kushadidi tishio dhidi ya “demokrasia” nchini Marekani.