Ripoti ya siri iliyotolewa na maafisa wa Idara ya Intelijensia ya Marekani imedai kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu umefanya jitihada kubwa za kujaribu kutatiza na kuvuruga mfumo wa kisiasa wa Marekani.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Baraza la Taifa la Intelijensia la Marekani imeeleza kuwa, kwa miaka mingi sasa, Imarati imetumia njia za kisheria na zisizo na kisheria kujaribu kupindisha sera za nje za Washington kwa maslahi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Gazeti la Washington Post limeripoti habari hiyo na kubainisha kuwa, tokea mwaka 2016 hadi sasa, UAE imetumia zaidi ya dola milioni 154 ‘kuwahonga’ wanafikra, Vyuo Vikuu na makundi ya kulobi ya Marekani ili yabuni magazeti na majarida yenye kupigia debe siasa na maslahi ya Imarati.
Ripoti hiyo ya Baraza la Taifa la Intelijensia la Marekani imeongeza kuwa, kitendo hicho cha Imarati cha kuingilia na kujaribu kuvuruga mfumo wa kisiasa wa Marekani hakina tofauti kubwa na vitendo vya ujasusi.
Baadhi ya Wabunge wa Marekani wamekosoa vitendo hivyo vya Umoja wa Falme za Kiarabu wakisisitiza kuwa, harakati hizo za Imarati zinaonesha namna ‘fedha za kigeni’ zinavyoweza kuingilia na kubadilisha siasa za ndani za Washington.
Ripoti hii imetolewa katika hali ambayo, Marekani imekuwa ikishirikiana na Imarati na Saudi Arabia katika jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu dhidi ya wananchi wa Yemen.