Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani kikao cha Rais wa Ufaransa na wapinzani wa Iran na kukitaja kitendo hicho kuwa ni ukiukaji mkubwa wa majukumu ya kimataifa ya Ufaransa katika kupambana na ugaidi na ukatili.
Katika wiki za hivi karibuni, maafisa wa utawala wa Ufaransa wameingilia wazi wazi masuala ya ndani ya Iran na kuunga mkono machafuko nchini, ambapo katika uchochezi wa hivi karibuni, siku ya Ijumaa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alikutana na kufanya mazungumzo na vinara wa wapinzani na mahasimu wa Iran mjini Paris.
Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran siku ya Jumapili alisema: “Inashangaza kwamba rais wa nchi inayodai kutetea uhuru anashusha hadhi yake anakutana na mtu kikaragosi anayechukiwa na ambaye katika miezi ya hivi karibuni amejaribu kueneza chuki na vitendo na kuchochea ghasia na ugaidi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mtu huyo pia amekuwa akihujumu maeneo ya kidiplomasia na wanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.”
Katika wiki chache zilizopita, serikali ya Ufaransa, sawa na nchi nyingine za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani na Uingereza, imeingilia wazi wazi masuala ya ndani ya Iran, na sasa inachukuliwa kuwa moja ya waungaji mkono wakuu wa machafuko na ghasia, sambamba na kuzidisha vikwazo vya kisiasa na kiuchumi dhidi ya Iran.
Kuhusiana na hili, siku ya Ijumaa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, katika uingiliaji wa wazi wa masuala ya Iran na kwa lengo la kuchochea machafuko nchini, alikutana na mwanamke anayejulikana kama Masih Alinejad, ambaye ni nembo ya uhasama na chuki dhidi ya Iran ambaye ana makao yake makuu huko New York. Machron alikutana pia na mahasimu wengine sugu wa Iran wakiwemo Laden Bromand, Shima Babaei na Roya Majidi katika Ikulu ya Elysee mjini Paris. Mkutano huo wa Macron na wapinzani sugu wa Iran umeungwa mkono na vyombo vya habari ajinabi na vyenye chuki na kinyongo dhidi ya Iran.
Mkutano huo ambao ulifanyika kwa juhudi za mahasimu sugu wa Iran na pia makundi yanayotaka kujitenga na Iran, unaonyesha kwa mara nyingine tena kwamba serikali ya Ufaransa, bila kujali wajibu wake wa kimataifa, inashirikiana na watu ambao wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kuzidisha machafuko na ghasia nchini Iran katika wiki za hivi karibuni. Kwa hivyo, mkutano huo unaweza kuchukuliwa kama kukuza vurugu na kukiuka majukumu ya serikali ya Ufaransa katika uwanja wa kupambana na ugaidi na ghasia.
Mbali na hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetoa tamko la uingiliaji kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Iran, ambapo mawaziri watatu washauri wa serikali ya nchi hiyo pia wameshiriki katika maandamano dhidi ya Iran mjini Paris. Ufaransa, pamoja na Ujerumani na nchi nyingine kadhaa za Ulaya pia, zinataka kuweka vikwazo zaidi vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran.
Ni wazi kuwa matukio ya hivi sasa yanaonesha tena misimamo na malengo ya nchi za Magharibi kama vile Ufaransa ambayo hadi sasa inadai kuwa inajaribu kufikia tamati ya mazungumzo ya Vienna kuhusu kuiondolea Iran vikwazo.
Nchi hizi za Ulaya zinajaribu kuendeleza machafuko nchini Iran na hatimaye kuyatumia kama kisingizio cha kuwekewa vikwazo vipya na mashinikizo zaidi Iran.
Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, iwapo Umoja wa Ulaya au nchi yoyote ya Ulaya itafuata mienendo ya uingiliaji, upendeleo na kutumia sera na misimamo ya kindumakuwili dhidi yake, basi Iran nayo itatoa jibu muafaka kwa uhasama huo.
Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdullahian, katika mazungumzo na baadhi ya washirika wa Ulaya, na Afisa wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kuwa hatua yoyote ya kiadui kutoka upande huo itakabiliwa na hatua sawia na inayofaa kutoka Iran.