Mapigano ya kikabila yaliyozuka katika eneo la Darfur huko Sudan yamesababisha vifo vya karibu watu 24 na kupelekea hali ya dharura kutangazwa eneo hilo.
Kiongozi mmoja wa kikabila ameziambia duru za habari kwamba, nyumba zimeteketezwa na mali kuporwa na hali bado inasalia kuwa tete hata baada ya kuwasili kwa maafisa wa usalama wa serikali.
Shirika la Habari la Sudan SUNA linasema kuwa, mamlaka nchini humo zimejaribu kuziomba pande husika katika mapigano hayo kusitisha uhasama ila juhudi hizo zimegonga mwamba. Machafuko yalianza mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya makabila mawili ya Kiarabu, kabila la Misseriya na Awlad Rashed karibu na eneo la Zanglei ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Darfur ya Kati. Kiongozi mmoja wa kabila la Misseriya amesema mzozo ulianza baada ya wizi wa pikipiki na kugeuka kuwa mapigano makubwa baina ya makabila mawili.
Sudan imeendelea kushuhudia mapigano na mauaji ya kikabila katika mbalimbali ya nchi hiyo na hivyo ukosefu wa usalama kuendelea kuwa tatizo kuu la nchi hiyo.
Mapigano hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, mwezi uliopita, watu wasiopungua 230 waliuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika mashambulizi ya dhidi ya vijiji kadhaa vya jimbo la Blue Nile, kusini magharibi mwa Sudan.
Mapigano haya ya hivi sasa ni wimbi jipya la ghasia za kikabila ambazo zimeenea kote nchini Sudan licha ya kutiwa saini mkataba wa amani wa nchi nzima miaka miwili iliyopita.
Wataalamu wanasema mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, yalizua ombwe la usalama ambalo limechochea kuibuka tena kwa ghasia za kikabila, katika nchi ambayo mapigano makali yanazuka mara kwa mara kuhusu ardhi, mifugo, upatikanaji wa maji na malisho.