Winnie Odinga, bintiye kiongozi wa Muungano wa Azimio, Raila Odinga, amesema kuwa nchi za Magharibi zilitumiwa kushawishi na kuyapa mwelekeo matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9.
Akizungumza katika Katika mahojiano na runinga ya Citizen, Winnie ameishutumu Marekani kwa kuingilia masuala ya kisiasa ya Kenya mara kwa mara kwa maslahi ya kibinafsi.
Binti huyo wa kiongozi wa upinzani wa Kenya amesema, madai ya mataifa ya Magharibi kuingilia uchaguzi wa Kenya ni ya kweli.
“Kenya ndiyo wanayoipenda zaidi. Ni PlayStation yao. Je, umewahi kuvaa miwani ya mchezo wa ukweli halisi? Hivyo ndivyo Kenya ilivyo kwao,” alisema Winnie Odinga.
Winnie ambaye ameteuliwa na chama cha ODM kwa ajili ya kugombea kiti cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA) amesema nchi za Magharibi zilihusika katika kuchakachua matokeo ya uchaguzi ikwa maslahi ya viongozi zinaowapendelea ili kulinda maslahi yao kwa gharimu ya Wakenya maskini.
Amesisitiza kuwa: “Nchi za Magharibi kwa miaka mingi zimekuwa zikiingilia masuala ya Afrika. Wanaingilia katika rasilimali na utawala wa Waafrika.”
Winnie Odinga pia ameishambulia Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani a nchi za Afrika na kusema: Kwa sasa Marekani imegawanyika. Hata hivyo badala ya Wamarekani kujishughulisha na masuala yao wenyewe, wanaingilia masuala ya bara la Afrika na wanachagua vitu au viongozi tofauti wa kuwekeza fedha zao kwao, na matokeo yake ni kuwaacha Waafrika katika umaskini wa kupindukia.”
Katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022 uliokuwa na ushindani mkubwa, William Ruto alipata kura milioni 7.18 (asilimia 50.49) dhidi ya kura milioni 6.94 za Raila Odinga (asilimia 48.85).