Chanjo tatu za aina adimu ya Ebola ziko tayari huku Uganda ikipambana na mripuko wa ugonjwa huo

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO amesema kwamba, chanjo tatu za aina adimu ya ugonjwa wa Ebola inayoendelea kusambaa hivi sasa nchini Uganda zitapelekwa nchini humo kwa majaribio ya kizahanati.

Dk. Matshidiso Moeti ameaambia waandishi wa habari kwamba chanjo hizo zitatumika katika mfumo unaojulikana kwa kimombo kama “ring vaccination trial” kwa maana ya kwamba, mbali na mgonjwa wa Ebola, watu waliokuwa na mawasiliano naye pia wote watapigwa chanjo.

Uganda imekuwa ikipambana na mripuko wa aina adimu ya virusi vya Ebola vilivyopewa jina la virusi vya Sudan. Hadi sasa hakuna chanjo ya kukabiliana na aina hiyo ya Ebola.

Akizungumzia mapambano ya ugonjwa huo hivi sasa huko Uganda, Dk. Fatuma Nakintu, afisa wa Wizara ya Afyaya Uganda amesema: “Tumeweza kuokoa maisha kwa kutoa huduma bora ya usaidizi hata bila ya chanjo iliyothibitishwa ya Ebola. Hii ni pamoja na kuwagundua mapema watu walioambukizwa na kutoa huduma ya haraka ya upungufu wa maji mwilini kwa kutumia viowevu vya IV na kutibu magonjwa mengine kama vile malaria.”

Akizungumza katika mkutano wa kilele wa G-20 mjini Bali, Indonesia, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kamati ya wataalamu wa nje imefanyia uchunguzi chanjo mbalimbali na kuamua kwamba chanjo hizo tatu zinapaswa kujumuishwa katika majaribio ya kliniki yaliyopangwa kufanyika nchini Uganda. Hata hivyo hakusema ni tarehe gani hasa zoezi hilo lingelifanyika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *