Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais Paul Kagame wa Rwanda wamekubaliana juu ya haja ya waasi wa M23 kusitisha mapigano na kuondoka katika maeneo waliyoyateka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hayoa yameelezwa kwenye taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Taarifa hiyo ya EAC imeongeza kuwa: Kenyatta na Kagame wote wamekubaliana katika mazungumzo waliyofanya kwa njia ya simu “juu ya hitajio la kusitisha mapigano mara moja”.
Wizara ya mambo ya nje ya Kenya imethibitisha pia kufanyika mazungumzo hayo kati ya Kagame na Kenyatta ambaye amekuwa akiongoza mazungumzo ya kuleta suluhu kati ya serikali ya Kinshasa na kundi la waasi wa M23.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, duru ya pili ya mazungumzo itafanyika wiki ijayo katika mji mkuu wa Angola, Luanda.
Vyombo vya habari vikiripoti kutoka mjini Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimesema, watu wa maeneo hayo wanasubiri kuona kama vikosi vya jeshi la serikali na vya waasi wa M23 vitasitisha mapigano baina yao.
Hii ni kutokana na kwamba pande hizo mbili zimekuwa zikipigana mpaka saa 24 zilizopita kukiwepo na ripoti za milio ya risasi inayosikika na mabomu ambayo bado yanaendelea kufyatuliwa. Kwa hiyo inasubiriwa kuona kama kweli vikosi vya pande mbili vitajiondoa katika maeneo hayo kabla ya mazungumzo ambayo yamepangwa kuanza Jumatatu asubuhi.
Katika wiki za karibuni, wapiganaji wa M23 wamepata mafanikio makubwa wakisonga mbele kuelekea Goma huku mapigano na vikosi vya serikali yakizidi kupamba moto.
Kundi la waasi wa M23 lilitia saini mkataba wa amani na serikali ya Kongo DR mwaka 2013 ambapo wapiganaji wake wengi walijumuishwa katika jeshi la serikali.
Hata hivyo kundi hilo lilianzisha mapigano tena mwishoni mwa 2021 baada ya kukaa kimya kwa miaka kadhaa.
Serikali ya Rwanda imekuwa ikituhumiwa na serikali ya DRC kuwa inawaunga mkono na hata kuwasaidia kijeshi waasi wa M23, tuhuma ambazo Kigali imekuwa ikizikanusha.
Mikwaruzano katika uhusiano wa nchi mbili ilishtadi mwezi uliopita baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumtimua balozi wa Rwanda nchini humo.