Nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Iran katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar amesema, vyombo vya habari vya Uingereza vimeanzisha mchezo wa vita vya kisaikolojia sambamba na kukaribia mechi kati ya timu ya nchi hiyo na Iran.
Timu ya taifa ya soka ya Iran imepangwa pamoja na Uingereza, Wales na Marekani katika Kundi B la Kombe la Dunia la Qatar 2022. Iran itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Uingereza Jumatatu Novemba 21.
Alireza Jahanbakhsh, nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Iran ameeleza hayo alipojibu swali la mwandishi wa habari aliyedadisi kuhusu hali ya siku hizi ndani ya Iran na kama matukio hayo yatakuwa na athari gani katika maandalizi ya timu ya taifa ya soka ya Iran, ambapo amesema, hashangai kuulizwa swali hilo na kwamba kila mmoja wao anasubiri kuulizwa suali kama hilo.
Jahanbakhsh ameeleza kuwa, kuna uwezekano mwandishi aliyeuliza suali hilo anatoka vyombo vya habari vya Uingereza na akaongeza kwamba, kama Iran na Uingereza zisingekuwa katika kundi moja, suali hilo lisingeulizwa.
Nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Iran amesisitiza kuwa vyombo vya habari vya Uingereza vimeanzisha mchezo wa vita vya kisaikolojia sambamba na kukaribia mechi katika ya timu ya nchi hiyo na Iran na akaeleza kwamba yeye na wachezaji wenzake wote wamejikita katika masuala ya soka tu, lengo lao pekee likiwa ni kuipa heshima jezi ya timu ya taifa na jukumu lao ni kucheza mpira.
Karim Ansari, mshambuliaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Iran, yeye amemwambia mwandishi wa habari wa Uingereza, “wewe andika vyovyote vile upendavyo kwa jibu lolote tutakalotoa”.