Waandamanaji wenye hasira wajaribu kuvamia ubalozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso

Polisi nchini Burkina Faso walirusha mabomu ya kutoa machozi siku ya Ijumaa kuwatawanya waandamanaji waliokuwa na hasira waliojaribu kuvamia ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu Ouagadougou, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.

Waandamanaji hao waliokuwa wakitaka balozi wa Ufaransa nchini humo atimuliwe, walikusanyika katika uwanja wa manispaa asubuhi kabla ya kuelekea kwenye ubalozi wa Ufaransa, ambako walitawanywa kwa mabomu ya kutoa machozi ya polisi.

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Le Faso,”Polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi baada ya mazungumzo na waandamanaji kuwataka kuondoka eneo la tukio kwa amani kushindwa kufikia natija. Waandamanaji walijibu kwa kuurushia mawe ubalozi.”

Waandamanaji hao baadaye waliripotiwa kuelekea Kamboinse, ambako kuna kambi ya kijeshi ya Ufaransa.

Picha za video zilionyesha waandamanaji hao, wengine wakiendesha pikipiki, wakipuliza firimbi na mavuvuzela wakipaza sauti wakisema “Mauti kwa Ufaransa.”

Waandamanaji, hasa vijana, wanaishutumu Ufaransa kuhusika katika matatizo ya Burkina Faso, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usalama.

Pia wanataka jeshi likatishe ushirikiano wa kiusalama na Ufaransa na badala yake wanataka nchi yao ianzishe uhusiano wa kijeshi na Russia.

Serikali ya Burkina Faso imetoa wito kwa wananchi na hasa vijana kujizuia na kutoibua ghasia wakati wa maandamano  dhidi ya Ufaransa,

Ikumbukwe kuwa, Ufaransa ina kikosi maalumu cha kijeshi nchini Burkina Faso, katika eneo la Kamboinse, kilomita 30 kutoka mji mkuu Ouagadougou.

Mwezi uliopita, waandamanaji wanaoipinga Ufaransa walijitokeza katika mji mkuu huku wakipeperusha bendera za Russia.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Januari ambayo yalimuondoa madarakani Rais  Roch Marc Christian Kabore, mwezi uliopita, wanajeshi waliokuwa na hasira wakiongozwa na Kapteni Ibrahim Traore walimtimua Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba katika mapinduzi ya pili ndani ya miezi minane.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *