Mashabiki wa soka wa nchi za Kiarabu wamekataa kuzungumza na waandishi wa habari wa masharika ya utawala haramu wa Israel nchini Qatar, kunakofanyika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu 2022; kuonyesha upinzani wao wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala huo bandia unaokaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, vijana wa Lebanon, Qatar na Saudi Arabia miongoni mwa nchi nyingine za Kiarabu walioko Qatar wamekataa kuhojiwa na wanahabari wa kanali ya 12 ya Kizayuni.
Mmoja wa maripota wa kanali ya 12 ya Israel amenukuliwa akisema, “Mashabiki karibu wote wa Kiarabu tuliokutana nao wamekataa kuzungumza nasi tulipojiarifisha na kuwaeleza kuwa tunatoka Israel.”
Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imeonesha kundi la vijana wa Lebanon wakikataa kuzungumza na wanahabari hao Wazayuni, baadhi wakiuwaliza, “Kwanza mnafanyaje hapa?”
Mmoja wa vijana wa Lebanon walioenda Qatar kutazama mechi za Kombe la Dunia zilizoanza jana amesikika kwenye kanda moja ya video akimuambia ripota wa Kizayuni katika eneo la Souq Waqif mjini Doha kwamba, “Hakuna kitu kama Israel, ni Palestina. Israel haipatikani.”
Vijana wengine kutoka Qatar na Saudia wameonekana kwenye video mitandaoni wakikataa kuzungumza na wanahabari hao wa utawala wa Kizayuni, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Wanamichezo mbalimbali wa nchi za Waislamu wakiwemo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisusia na kukataa kucheza na kukabiliana na Wazayuni katika michezo na mashindano mbalimbali.