Wanachama wa genge moja la kigaidi wameshambulia kambi ya jeshi na mji mmoja huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua idadi kubwa ya raia na maafisa usalama.
Duru za kiusalama zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, mashambulio hayo yanayoaminika kufanywa na wanamgambo wa kundi la kigadi la ISIS Wilaya ya Afrika Magharibi (ISWAP) yameua wanajeshi tisa, askari polisi wawili na raia kadhaa katika mji wa Malam Fatori, wilaya ya Abadam, kaskazini mashariki mwa nchi.
Idadi ya raia waliouawa katika mashambulizi hayo yaliyoanza tangu Ijumaa iliyopita haijajulikana. Mmoja wa wakazi wa mji wa Malam Fatori, Buji Garwa amesema, “Idadi ya raia waliouawa haijulikani kwa sababu sote tulikimbia. Sehemu kubwa ya mji umechomwa moto.”
Mkazi mwingine wa mji huo, Baitu Madari amesema binafsi ameshuhudia makumi ya maiti zimetapakaa katika vijiji vya mji huo baada ya kutokea mashambulio hayo.
Habari zaidi zinasema kuwa, wanachama hao wanaosadikika kuwa wa ISWAP walitoka katika kijiji cha Kamuya, umbali wa kilomita 8 kutoka mji wa Malam Fatori, ulioko yapata kilomita 200 kutoka Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu wasiopungua 12 kuuawa katika shambulizi jingine la kigaidi huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Ukosefu wa usalama umeongezeka nchini Nigeria hivi sasa wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikikaribia kwenye Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Februari mwaka ujao 2023.