Saudia imeua Wayemen 18,000, kuharibu misikiti 1,679 tokea 2015

Shirika moja la kutetea haki za binadamu limesema watu zaidi ya 18,000 wa Yemen wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa Saudi Arabia katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu mwaka 2015.

Kituo cha Humanity Eye Centre for Rights and Development kimesema katika ripoti yake mpya kuwa, idadi jumla ya wahanga imefikia 47,673 katika siku 2,800 za mashambulizi hayo.

Ripoti ya kituo hicho cha haki za binadamu imeeleza kuwa, mbali na Wayemen 18,013 kuuawa katika mashambulizi hayo ya askari vamizi, wengine zaidi ya 29,660 wamejeruhiwa.

Humanity Eye Centre for Rights and Development imeeleza kuwa, watoto 4,061 ni miongoni mwa wananchi wa Yemen waliouawa kufikia sasa katika mashambulizi hayo, huku wengine 4,739 wakijeruhiwa.

Aidha kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, wanawake 2,454 wameuawa katika kipindi cha miaka minane ya hujuma za kila upande za muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen, mbali na 2,966 kujeruhiwa.

Ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imeeleza kuwa, hujuma hizo zimeharibu nyumba 598,000, Vyuo Vikuu 182, Misikiti 1,679, vituo vya utalii 379 na hospitali na vituo vya afya vipatavyo 415.

Hivi karibuni Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ilitangaza kuwa, zaidi ya watoto elfu 4 wa Yemen wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, wengine 4,588 wamejeruhiwa, huku watoto milioni 2.4 kati ya watoto wapatao milioni 10 walio na umri wa kwenda shule wa Yemen, wakikoseshwa elimu na mzingiro na hujuma hizo.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *