Wananchi wa Afrika Mashariki wana wasi wasi mkubwa kutokana na makadirio ya kushuka kwa uchumi duniani mwaka 2023 baada ya Shirika la Fedha Duniani kutangaza kuwa karibu theluthi moja ya dunia itadorora kiuchumi, ikiongozwa na mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani ikiwa ni pamoja na Marekani, China na Ulaya.
Makadirio ya hivi majuzi yanaweka matarajio ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka huu na ujao kuwa bora kuliko wastani wa kimataifa, lakini wachambuzi wanasema kanda hiyo haiwezi kuepuka mdororo unaokuja.
Kulingana na ripoti ya Mtazamo wa Kiuchumi wa Dunia wa IMF iliyotolewa mwezi uliopita, kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa kitashuka kutoka asilimia sita mwaka jana hadi asilimia 3.2 mwaka 2022, na kushuka zaidi hadi asilimia 2.7 mwaka 2023 kutokana na usumbufu uliosababishwa na mzozo wa Ulaya Mashariki.
Uchumi wa Afrika Mashariki, hata hivyo, unatabiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 mwaka huu, ukishuka kutoka asilimia 6.4 mwaka jana, lakini unatarajiwa kuimarika hadi asilimia 5.6 mwaka ujao, jambo linaloangazia utendaji bora kuliko mataifa mengine duniani.
Lakini pamoja na hayo, wanauchumi na wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema wananchi watahitaji kukabili nyakati ngumu za kiuchumi mwaka ujao kwani mdororo unaokuja unaweza kusababisha upungufu wa nafasi za ajira, kupunguzwa kwa mishahara, na kuzorota kwa jumla kwa shughuli za kiuchumi na kutatiza maisha.
Ken Gichinga, mwanauchumi mkuu katika kampuni ya Kenya ya uchanganuzi ya Mentoria Economics, anakubali kwamba Nairobi na maeneo mengine ya Afrika Mashariki huenda yakakumbwa na mdororo wa kiuchumu mwaka ujao, lakini hali haitakuwa mbaya kama itakavyokuwa katika masoko ya nchi zilizostawi.
Macho sasa yanaelekezwa kwa watunga sera watakavyotumia mbinu bora zaidi za kuleta utulivu wa uchumi ili kupunguza athari za mdororo wa uchumi unaokuja na kusaidia kuokoa kazi na riziki kwani mdororo unaokuja unazua hofu.