Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema linatiwa wasiwasi na kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Tor Wennesland Mratibu Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani katika eneo la Asia Magharibi amebainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kuongezeka hatua za kuwabana Wapalestina katika ardhi hizo na kutangaza kuwa: mashambulizi na hujuma za utumiaji mabavu yanayofanywa na walowezi wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina katika mji wa al Khalil kwa mara nyingine tena yatashadidisha pakubwa mapigano.
Dmitriy Polyanskiy Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia Umoja wa Mataifa pia amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba: amesikitishwa kuona kwamba kadhia muhimu ya Palestina imewekwa kando kwa sababu ya maslahi ya Marekani na waitifaki wake. Ameongeza kuwa, mwaka huu wa 2022 zaidi ya Wapalestina 130 wameuawa katika oparesheni za kijeshi za Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ghaza. Amesema, kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, Wapalestna kuporwa ardhi zao, kubomolewa nyumba zao na kutiwa nguvuni kiholela raia hao ni hatua ambazo zimeifanya hali ya Wapalestina kuwa ngumu sana.
Mwakilishi huyo wa Russia katika kikao cha Baraza la Usalama amelaani na kukosoa vikali pia hatua ya utawala wa Israel ya kukiuka mamlaka ya kujitawala na kuzishambulia Syria na Lebanon; vitendo ambavyo vinafanyika chini ya kimay cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika kipindi cha nusu karne iliyopita, Marekani imeyapigia kura ya turufu maazimio 35 yaayoihusu Palestina katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.